Tuesday, September 6, 2016

MFAHAMU RAISI WA UFILIPINO RODRIGO DUTERTE, KIONGOZI ALIEMTUSI OBAMA.



Rodrigo "Digong" Duterte ni kiongozi ambaye msimamo wake na matamshi yake huzua utata mara kwa mara. Amegonga vichwa vya habari tena baada ya kuonekana kumtusi Rais wa Marekani Barack Obama na kumuita "mwana wa kahaba".
Duterte aliweza kukabiliana na utata juu yake na kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Ufilipino wa mwezi Mei.
Baada ya kula kiapo cha urais, Juni 30 Bw Duterte, ambaye kipindi kirefu aliishi mjini Davao kusini mwa nchi tangu aliposhinda, ana mamlaka ya kuongoza taifa hilo kwa muhula mmoja wa miaka sita.
Rodrigo "Digong" Duterte alizaliwa mnamo mwaka 1945 katika familia iliyojikita katika siasa za ndani ya nchi.
Wakati mmoja baba yake alikuwa gavana wa jimbo, na familia hiyo ilikuwa na uhusiano na familia zenye ushawishi mkubwa za Duranos na Almendrases katika jimbo Cebu, ambako baba yake aliwahi kuwa meya.
Bw Duterte amesomea taaluma ya sheria na alipanda cheo hadi kuwa mwendesha mashtaka kabla ya kuteuliwa kuwa naibu meya wa Davao wakati wa mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Ferdinand Marcos mwaka 1986.
Alikuwa meya mwaka 1988 na kushikilia wadhfa huo kwa kipindi cha miaka 10, kabla ya kushinda kiti cha ubunge katika Bunge la Congress halafu akarejea kwenye kiti cha umeya mwaka 2001.
Duterte ambaye utawala wake ni wa kipekee kwa kuwa kiongozi mwenye sera za Kijamaa na mwanamageuzi kwa pamoja, sera zake za uchumi zilikuwa si za kuaminika wakati wa kapeni.


Alijijengea umaarufu kwa kupiga vita baadhi ya matatizo makubwa yanayowakabili Wafilipino - uhalifu, makundi ya uasi, na ufisadi. Yote haya yalipungua kwa kiwango kikubwa wakati alipokuwa kiongozi wa Davao, na kufanya mji huo kuwa mmoja wa miji salama zaidi nchini Ufilipino.

Kuzua utata mkubwa

Aliahidi kubadili mfumo wa utawala wa taifa kutoka kwa mfumo wa bunge moja kuu yenye hadi kwenye mabunge ya majimbo, ili kugawana vyema mali ya taifa.
Msemaji wake alisema kutakuwa na "mageuzi makubwa yatakayofanyiwa katiba ya nchi".
Pia alikuwa ameahidi "kuwaua wahalifu 100,000" akiingia ikulu ya rais, akiongeza kuwa angepatia vikosi vya usalama uwezo wa "kupiga risasi na kuuwa" washukiwa wanaokwepa kukamatwa.
Tayari kufikia sasa, washukiwa 2,5000 wameuawa.
Ili kutekeleza baadhi ya mipango yake, atahitajika kuungwa mkono na kupata idhini kutoka kwa Bunge la Congress.

Kutusi watu

Amewahi kutangaza hadharani kwamba Ufilipino, ambayo imekuwa mshirika mkuu wa Marekani, haitategemea sana Washington.
Kijamii, yeye huunga mkono wapenzi wa jinsia moja lakini ni mhafidhina katika masuala mengi ya kijamii. Amegusia kupiga marufuku unywaji pombe maeneo ya wazi na kutoa amri ya kutotoka nje kwa vijana.
Amekuwa akiwatusi watu mashuhuri. Alimwita Papa Francis "mwana wa kahaba" (Ufilipino ni taifa lenye Wakatoliki wengi). Amewahi kumtusi pia waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kwa kumuita "mwendawazimu" na majuzi alimweleza balozi wa Marekani nchini Ufilipino kama "mpenzi wa jinsia moja ambaye ni mwana wa kahaba".

Alifanya mzaha na kusema kwamba alipokuwa meya angekuwa mtu wa kwanza kumbaka mmishenari kutoka Australia aliyeuawa wakati wa fujo gerezani.
Msimamo wake mkali umemfanya abandikwe majina ya "mtoa adhabu " na "Duterte Harry".

Kuwaua wanawe

Alisema kwenye mdahalo wa televisheni kwamba anaweza kuwauwa wanawe kama watatumia mihadarati.
Yote hayo yamemuongezea sifa miongoni mwa wengi nchini Ufilipino kama mtu anayeweza kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha mambo muhimu yanatekelezwa .
Amekuwa akilinganishwa na mgombea wa urasi wa Marekani Donald Trump, lakini alikataa kufananishwa naye, akisema kwamba Trump "hakubali maoni ya wengine, lakini mimi sivyo".
Bw Duterte ameoa mara mbili, ana watoto wanne, na miongoni mwao binti yake Sara - alikuwa meya kwa muhula mmoja kabla ya kurejea tena kwa baba yake .
Kwa sasa hana mke, lakini anadai kuwa na marafiki kadhaa wa kike.
(HABARI KWA HISANI YA BBC).

TAARIFA YA SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO KUHUSU RAIS MAGUFULI KUPITISHA MISWADA MITANO



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameridhia na kusaini Miswada mitano kutumika kama Sheria kamili za nchi.

Hayo yamesemwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai mara baada ya kufungua Mkutano wa nne wa Bunge la 11 leo mjini Dodoma.

Miswada iliyoidhinishwa na Rais ni pamoja Sheria ya Fedha na Matumizi ya mwaka 2016, Sheria ya Fedha namba 2 ya mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2016, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbambali namba 2 na 4 ya mwaka 2016 na Sheria ya Marekebisho ya Ununuzi ya Umma namba 5 ya mwaka 2016.

Aidha, Mhe. Spika amewakumbusha Wabunge kusoma na kuelewa kila kinachokuja Bungeni ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kibunge ipasavyo kwa niaba ya wananchi waliowatuma kufanya kazi hiyo ili kuwaletea maendeleo.

Wabunge wametakiwa kutekeleza majukumu hayo ya uwakilishi wa wananchi ili waweze kujadili masuala mbalimbali kwa kuzingatia haki, ustahimilivu, busara, hekima na kutumia lugha ya staha katika mijadala ya Bunge.

Vile vile Mhe. Spika amempongeza Naibu Spika Dkt. Tulia Akson kuongoza vema mkutano wa tatu wa Bunge ulioanza Aprili 19 na kumalizika Juni 30 mwaka huu kwa kushirikiana na wenyeviti wa Bunge Andrew Chenge, Mussa A. Zungu na Najima Giga.

Katika hatua nyingine Mhe. Spika amemshukuru Rais Dkt. Magufuli, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote walimuombea alipokuwa kwenye matibabu nje ya nchi pamoja na Madaktari waliomhudumia akiwa kwenye matibabu na kumshukuru Mungu kwa kumwonesha upendo alipokuwa kwenye mapito ya kuugua.

Katika mkutano huo wa Bunge yameulizwa maswali 14 ambayo yalielekezwa kwenye Wizara mbalimbali na kujibiwa kwa llengo la kutolea ufafanuzi masuala yanayotekelezwa kwa Serikali.

ACT-WAZALENDO WATOA TAMKO RASMI KUHUSU HALI YA NCHI KWA SASA



Tamko Rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo kuhusu HALI YA NCHI
Dar Es salaa, Jumanne, 06 Septemba 2016
1. Utangulizi
Jana Jumatatu, 5 Septemba 2016, Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo ilikutana katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kuidhinisha Taarifa kuhusu HALI YA NCHI. Taarifa hii sasa inatolewa rasmi kwa umma. Taarifa ipo katika maeneo makubwa manne: Hali ya kisiasa, hali ya kiuchumi, umoja wa kitaifa na hitimisho.
2. Hali ya Kisiasa
Kamati Kuu imezingatia kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeanisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Hata hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kuzuia shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na hata Jeshi la Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani inapaswa kukoma mapema baada ya uchaguzi. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi. Kisiasa, tunatambua kwamba Viongozi wa CCM wamepoteza mvuto kwa wananchi na sasa wanamsukuma Mwenyekiti wao Rais Magufuli kutumia jeshi katika kuokoa taswira ya Chama cha Mapinduzi mbele ya umma.
Kwa kuzingatia hali ya kisiasa nchini kwa sasa, Kamati Kuu ya chama chetu:
i) Tunalaani na kupinga kwa nguvu zetu zote hatua za Serikali ya Chama cha Mapinduzi za kuvunja Katiba na kujaribu kuweka pembeni utawala wa sheria.
ii) Tunapinga vitendo vinavyozidi kushamiri katika serikali hii ya CCM ya kujaribu kuendesha nchi kwa ubabe na matamko ya viongozi badala ya utawala wa sharia.
iii) Tutasimama imara, na tutaungana na vyama vingine vya siasa pamoja na taasisi zingine za kiraia katika kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, uhuru wa maoni, na utawala wa sheria katika nchi yetu
3. Hali ya Kiuchumi
Katika miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu imejenga uchumi ambao umekuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hiki. Ukuaji huu wa uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na kuchochea shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipata cha chini. Awamu ya tano ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi imerithi changamoto ya uchumi unaokua bila kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Hili ndilo tulitegemea Serikali mpya ishughulike nalo.
Kamati Kuu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi katika kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano. Kwa mfano:
a) Taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba – Desemba 2015 ) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari – Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli umepungua kwa 4%.
b) Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. Hii ina maanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani
c) Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilikuwa 13.8% lakini ukuaji wa sekta hii katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka.
d) Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji itaathiri watu wengi, wakiwemo madereva, matingo, pamoja na mama Ntilie wanaowauzia chakula. .
Kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, Kamati Kuu:
a) Tunaitaka serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha uchumi wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa washauri wa uchumi itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi.
b) Inahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa sheria. Juhudi za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua uwekezaji na kuangamiza uchumi wa nchi. Tusirihusu CCM iue uchumi wa nchi kwa maslahi yake ya kisiasa na viongozi wake.
4. Umoja wa Kitaifa
Nchi yetu imefanya juhudi kubwa katika miaka 50 iliyopita katika kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha kuwa makabila, dini na baadaye vyama vya siasa tunaishi bila kukamiana. Juhudi za dhati za kupambana na ubaguzi ndiyo umekuwa msingi imara wa kujenga Umoja wa Kitaifa na amani tunayojivunia.
Hata hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa utawala mpya wa Serikali ya CCM, kupitia Mwenyekiti wake mpya na Rais wa Jamhuri wa Muungo, umeanza kwa juhudi na kasi kubwa kuchokonoa na kumomonyoa misingi ya utaifa na umoja wetu. Sasa tunaye Rais asiyechagua maneno na asiyejua aongee nini na wapi. Vijana waliosoma kwa bidii katika mazingira ya shule zilizotelekezwa na serikali ya CCM anawaita VILAZA. Katikati ya uhasama mkubwa wa kisiasa na kijamii huko Zanzibar Rais wetu amefunga safari, sio kujaribu kutibu majeraha yaliyosababishwa na kuchezewa kwa sanduku la kura, bali kuchochea uhasama chini ya ulinzi wa vyombo vyetu vya dola vyenye jukumu la kulinda na kudumisha amani. Sasa Rais wetu, kupitia kauli zake, ameanza kuubomoa muungano wetu uliojengwa kwa unyenyekevu na katika mazingira magumu. Kila asimamapo kuhutubia, jambo moja la kutarajiwa kutoka katika kinywa cha Rais wetu ni matamshi yanayodhoofisha nguzo fulani ya umoja, mshikamano na undugu wetu kama taifa. Yote haya yakitokea chama chake cha CCM ama kimekaa kimya au kinachekelea. Inasikitikitisha kwamba Chama kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere kinamruhusu kiongozi wake kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na kuchochea chuki katika jamii ya watanzania.
Kwa kuzingatia mtikisiko mkubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa unaoendelea nchini, Kamati Kuu:
a) Tunalaani juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Mwenyekiti wao za kuchochea chuki katika jamii ya watanzania na kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na amani ya nchi
b) Tunatoa wito kwa watanzania wote waipendayo nchi yao kusimama kidete katika kulinda misingi ya nchi yetu na kukataa chuki inayoanza kujengwa na utawala wa CCM
c) Tunatoa wito wa kipekee kwa viongozi wetu wa dini na wakuu wa nchi waliopita, hususani Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na wazee wengine wanaoheshimika katika nchi yetu wavae ujasiri wa kumuonya Mwenyekiti wa CCM kuwa juhudi zake za kuchochea chuki katika jamii yetu ya watanzania zitasambaratisha Taifa letu.
5. Hitimisho
i) Sisi kama chama cha siasa, tunaendelea kusisitiza kuwa tutaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi na kujenga uwajibikaji nchini.
ii) Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuheshimu na kulinda demokrasia na kuzingatia utawala wa sheria nidyo msingi wa mapambano dhidi ya ufisadi. Tunasisitiza kuwa mtu yeyote, wa kawaida au kiongozi, anayesema kwamba anaweza akapambana na ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na utawala wa sheria mtu huyo ni mwomgo na kwa kweli ni fisadi na anataka kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu huyo, pamoja na mambo yake yote, yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka!
iii) Tunasisitiza kuwa msingi wa uchumi wetu ni kuvutia uwekezaji wa ndani nan je ya nchi. Kuzingatia utawala wa sheria ndiyo msingi wa kuvutia uwekezaji. Juhuzi za hivi karibuni za serikali ya CCM za kujaribu kuua utawala wa sharia ni juhudi ovu za kuua uchumi wa nchi yetu. TUZIKATAE juhudi za kuua utawala wa sheria kwa kuwa zitaangamiza taifa letu kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
Dar es Salaam, Jumanne 6 Septemba 2016.

Monday, September 5, 2016

JINSI MAJAMBAZI WALIVYOULIWA NA MWENZAO HAPO JUZI


Baada ya jeshi la Polisi kufanya msako mkali kuanzia Tar 3 Septemba, walifanikiwa kukamata majambazi sugu wakiwa na shehena ya silaha za kivita. Na baada ya mahojiano majambazi hao walikiri kuwa wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Ndipo askari walifuatana na watuhumiwa hao hadi kwenye msitu wa Vikindu.

Alisema askari walipofika eneo hilo, walilodai ni karibu na zilipo silaha hizo, walishuka kwenye gari na kuingia porini wakiwa wamewatanguliza watuhumiwa mbele majira ya usiku.

Aliongeza kuwa wakiwa msituni humo na askari wakiwa wenye tahadhari kubwa, ghafla walisikia milio ya risasi ikitokea mbele, ambapo askari walilala chini na baadaye zikisikika sauti zikisema ‘mmetuua sisi’.

Alisema baada ya risasi za mfululizo kutulia, askari walishuhudia majambazi hao ambao walichelewa kulala chini wakati risasi zikipigwa wakiwa wamejeruhiwa sehemu za kifuani na tumboni huku wakivuja damu nyingi.

Alisema askari walipiga risasi kuelekeza eneo zilikotokea risasi na walipoendelea kusonga mbele, walikuta silaha aina ya SMG ikiwa imetelekezwa na haikuwa na risasi ndani ya magazine, hivyo kufanya idadi ya silaha za SMG kufikia nne.

Aidha alisema askari waliwabeba majambazi hao na kuwapeleka kwenye gari kuelekea hospitalini, lakini wote walifariki dunia wakiwa njiani kutokana na kutoka damu nyingi. 

Akizungumzia tukio la Vikindu, Sirro alisema wamefanikiwa kuwakamata watu hao wanaosadikiwa kuhusika na tukio ambalo lilisababisha kifo cha askari mmoja.

“Majambazi hao walikuwa ni kundi la kama watu 14 na tayari tumewakamata zaidi ya saba ambao mpaka sasa tunawashikilia kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha upelelezi,” alisema Kamanda Sirro.

Pia alisema kumekuwa na taarifa mbalimbali, zikisambazwa katika vyombo vya habari zikidai kuwa katika tukio la Vikindu, kuna askari anahusika na tukio hilo na kudai taarifa hizo si za kweli na hakuna askari aliyehusika katika tukio hilo.

Katika tukio lingine, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa makosa ya wizi wa magari manane, likiwemo gari moja la kibalozi. 

Kamanda Sirro alisema magari hayo yaliibwa jijini Dar es Salaam na kuuzwa kwa watu mbalimbali jijini hapo na mikoani na watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Sirro alisema katika tukio lingine jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wanaodaiwa kuhusika na kuvunja nyumba usiku na kuiba. 

Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

WAZIRI MKUU MH MAJALIWA LEO AMEKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA SPIKA WA BUNGE, BWANA JOB NDUGAI



Ikiwa imesalia siku moja kabla ya mkutano wa nne wa bunge la kumi na moja kuanza hapo kesho September 6 2016 leo Waziri  Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Spika wa bunge Job Ndugai pamoja na viongozi wengine katika ofisi za bunge zilizopo Dodoma kwa lengo la kufanya kikao cha maridhiano ya vyama vyote.

NAIBU WAZIRI TAMISEMI APATA AJALI YA GARI

Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo amepata ajali eneo la Katela Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe Mbeya.


Ajali hiyo imehusisha gari dogo aina ta Corola iliyokuwa ikotokea Mbeya kwenda Rungwe na Naibu Waziri Selemani Jafo alikuwa akitokea Tukuyu kikazi.

Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja amesema katika gari Waziri walikuwa watatu, Waziri Jafo mwenyewe Katibu wake na Dereva na wote walitoka salama katila ajali hiyo.

Alisema baada ya kupata ajali hiyo walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya ambapo walifanya uchunguzi kama wameumia kwa ndan au laa! Lakin bahat nzuri Daktari aliyewafanyia uchunguz alisema hakuumia popote ni wazima.

Alisema baada ya hapo Waziri na watu waliendelea na safari yao kuelekea mjini Dodoma kwa ajili ya kuwahi vikao vya Bunge

MAJAMBAZI YANASWA NA SHEHENA YA SILAHA ZA MOTO



Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wanadaiwa kukamatwa na polisi wakiwa na zana mbalimbali ambazo hutumiwa na vyombo vya ulinzi zikiwamo silaha za vita na sare za polisi.

Vitu hivyo vinadaiwa kutumiwa na watu hao kufanya   ujambazi.Inadaiwa kwamba watu hao ni wale waliovamia na kuiba fedha katika jengo la Sophia House lililopo Keko   Dar es Salam wakiwa wamevaa sare za polisi na kutumia gari   ya Noah.

Taarifa  kutoka chanzo cha kuaminika zinaeleza kwamba watu hao ni pamoja na mwanamke mmoja aliyekamatiwa   Bunju  katika Manispaa ya Kinondoni ambako vilikutwa vitu vyote vilivyoporwa na wanaume wawili waliokamatiwa   Mbagala Manispaa ya Temeke,   Dar es Salaam.

Chanzo hicho kilieleza kwamba silaha zilizokamatwa  ni pamoja na bunduki tatu za SMG na risasi zake 260, bastola 16 na risasi zake 526, panga moja na michimbiko mitatu ya kung’olea mageti..

Vitu vingine ni   pingu za chuma 45 na tatu za plastiki, ‘radio call’  12 , kamera ya CCTV moja, gari moja   ya Noah, sare ya polisi jozi moja, ‘pump action tatu na mkasi mmoja.