Monday, September 5, 2016

JINSI MAJAMBAZI WALIVYOULIWA NA MWENZAO HAPO JUZI


Baada ya jeshi la Polisi kufanya msako mkali kuanzia Tar 3 Septemba, walifanikiwa kukamata majambazi sugu wakiwa na shehena ya silaha za kivita. Na baada ya mahojiano majambazi hao walikiri kuwa wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Ndipo askari walifuatana na watuhumiwa hao hadi kwenye msitu wa Vikindu.

Alisema askari walipofika eneo hilo, walilodai ni karibu na zilipo silaha hizo, walishuka kwenye gari na kuingia porini wakiwa wamewatanguliza watuhumiwa mbele majira ya usiku.

Aliongeza kuwa wakiwa msituni humo na askari wakiwa wenye tahadhari kubwa, ghafla walisikia milio ya risasi ikitokea mbele, ambapo askari walilala chini na baadaye zikisikika sauti zikisema ‘mmetuua sisi’.

Alisema baada ya risasi za mfululizo kutulia, askari walishuhudia majambazi hao ambao walichelewa kulala chini wakati risasi zikipigwa wakiwa wamejeruhiwa sehemu za kifuani na tumboni huku wakivuja damu nyingi.

Alisema askari walipiga risasi kuelekeza eneo zilikotokea risasi na walipoendelea kusonga mbele, walikuta silaha aina ya SMG ikiwa imetelekezwa na haikuwa na risasi ndani ya magazine, hivyo kufanya idadi ya silaha za SMG kufikia nne.

Aidha alisema askari waliwabeba majambazi hao na kuwapeleka kwenye gari kuelekea hospitalini, lakini wote walifariki dunia wakiwa njiani kutokana na kutoka damu nyingi. 

Akizungumzia tukio la Vikindu, Sirro alisema wamefanikiwa kuwakamata watu hao wanaosadikiwa kuhusika na tukio ambalo lilisababisha kifo cha askari mmoja.

“Majambazi hao walikuwa ni kundi la kama watu 14 na tayari tumewakamata zaidi ya saba ambao mpaka sasa tunawashikilia kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha upelelezi,” alisema Kamanda Sirro.

Pia alisema kumekuwa na taarifa mbalimbali, zikisambazwa katika vyombo vya habari zikidai kuwa katika tukio la Vikindu, kuna askari anahusika na tukio hilo na kudai taarifa hizo si za kweli na hakuna askari aliyehusika katika tukio hilo.

Katika tukio lingine, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa makosa ya wizi wa magari manane, likiwemo gari moja la kibalozi. 

Kamanda Sirro alisema magari hayo yaliibwa jijini Dar es Salaam na kuuzwa kwa watu mbalimbali jijini hapo na mikoani na watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Sirro alisema katika tukio lingine jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wanaodaiwa kuhusika na kuvunja nyumba usiku na kuiba. 

Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment